Muziki hauna dini, umri, jinsi, kabila wala itikadi vivyo hivyo katika sanaa ya uigizaji. Bado wengi wanajiuliza maana halisi ya muziki, lakini Kamusi Sanifu ya Kiswahili imeeleza kuwa ni muziki ni mpangilio wa ala na uimbaji unaoleta athari fulani kwa kiumbe.
Hivyo, athari zitokanazo na muziki huburudisha, huhamasisha, huondoa msongo wa mawazo pia huelimisha.
Hapa kwetu muziki unatumika katika sekta nyingi na wasanii wamekuwa radhi hata kubadilisha hakimiliki ya kazi zao na kuzivisha maneno ya vyama vya kisiasa zikatumika katika kampeni.
Wakati nchini Tanzania kampeni za kisiasa zikiwa zimepamba moto, wasanii nao wamejiingiza katika ushabiki wa masuala hayo, hii ni tofauti na miaka ya zamani kwani wameamua kujipambanua kwa kuweka wazi matakwa na mapenzi yao kisiasa.
Mwanamuziki wa kiume anayekubalika na kutambulika nje ya bara la Afrika, Diamond Platnumz anaamini kwamba kila Mtanzania anahusika kuchagua kiongozi anayeamini kwamba ni bora na kwake hasiti kutangaza nani anamshabikia.
“Kwa Uchunguzi na tathmini niliyoifanya tangu kampeni zianze, nimegundua na kuamini kuwa mgombea urais John Magufuli ndiyo jembe. Nimeamua kumshabikia tena waziwazi bila kificho. Mashabiki wangu wataamua ila siwezi kubadili kazi zangu, naingiza fedha kupitia kazi hii pia,” alisema Diamond.
Rapa wa muziki wa kizazi kipya ambaye pia ni mtangazaji, Soggy Doggy ameweka wazi kwamba kuna faida na hasara za msanii kujiingiza katika siasa na kuweka wazi kwamba yeye ni mwanasiasa na aliye upande wa Ukawa.
“Nimeamua kuvaa mabomu. Naamini kwa ninachokipigania kwamba ni kizuri na naamini Ukawa tukishinda itakuwa ni faida kubwa kwangu. Lakini kuna hasara ikiwa itapoteza hata sasa najua wapenzi wa muziki wanajigawa na hiyo ndiyo iliyomfanya msanii Marlaw akapotea katika ulingo wa siasa,” alisema Soggy Doggy.
Licha ya wasanii wa muziki, waigizaji hasa wa kike wameonekana kuwa na mwamko mkubwa kujihusisha katika siasa miaka ya hivi karibuni, Wema Sepetu ambaye ni kiongozi wa vuguvugu la kampeni kwa wasanii kupitia Chama cha Mapinduzi, anasema hajaingia kutafuta pesa wala umaarufu kwani hivyo vyote anavyo tayari.
“Naipenda Tanzania yangu na najua baada ya muda mfupi nitaipenda zaidi, mimi ni mkereketwa haswa mikoba nimeachiwa na mzee wangu, sihami ng’o nimeingia huku kwa kuwa ni kitu ninachokipenda lazima niwe muwazi hata kwa mashabiki wangu,” anasema Wema.
Mwigizaji Jacqueline Wolper, anayeongoza vuguvugu la kampeni za Chadema chini ya Ukawa, amesema kuingia kwake katika hamasa ndani ya Chadema si kusaka uongozi bali anahitaji mabadiliko na ana haki kikatiba.
“Sisi kama wasanii tuna nafasi yetu katika mchakato huu wa kisiasa, lazima tuonyeshe tunahitaji nini na mtu sahihi kwa sasa ambaye anaweza kuleta mabadiliko,” anasema. Wolper anasema amegundua wasanii wanatumika katika kampeni kila uchaguzi unapokuja lakini baada ya kampeni kumalizika hakuna kinachoendelea, bali kuna watu wanaojinufaisha wao kwa mgongo wa wasanii.
Mwanamuziki mkongwe na mchambuzi wa masuala ya sanaa nchini John Kitime, anasema licha ya wasanii wengi kujipambanua hivi sasa walio wengi wanaangalia zaidi faida zitokanazo na masuala ya kampeni za kisiasa pasipo kung’amua hasara zake baadaye.
Kitime anasema miaka ya 70 mpaka 80 wasanii walio wengi ilikuwa ni lazima wawe na kadi za chama cha Tanuna hata baadaye ilivyokuja CCM, hiyo iliwasaidia wao kujihusisha na masuala ya kisiasa na hata kuweza kufungulia akaunti benki, kibali cha kuandaa onyesho, pia ilikuwa ni kadi ya chama.
“Kwetu ilikuwa ni kama kitambulisho, kwa maana hakukuwa na chaguo la ziada ilitulazimu kuwa huko na hata tulitumbuiza kwa kuwa wananchio wote walikuwa katika chama kimoja. Hakuna mtu ambaye alikuwa anazifikiria hasara za upande wa pili, tulishiriki katika masuala ya Mwenge wa Uhuru, sherehe mbalimbali za kitaifa yaani kadi ilituwezesha hivi vyote,” anasema Kitime.
Wasiwasi wa Kitime leo unakuja kwa kile alichokiita demokrasia, anasema vyama vingi vimekuwepo miaka ya sasa na kila kimojawapo kinafikiria namna msanii atakavyoweza kukinufaisha.
Anasema haijalishi ni mwimbaji au mwigizaji bali ni namna atakavyoleta ushawishi wake katika jambo analotaka kulifanya.
Kitime anasema ikiwa demokrasia ya nchi bado ni changa, walio wengi wanawafikiria tofauti walio katika mlengo wa chama tofauti na wao na hivyo kujenga chuki, msanii akishiriki katika chama ambacho yeye hashabikii anakuwa adui yake. “Hasara zilizopo kwa msanii ni kupoteza mashabiki kwa kuwa demokrasia yetu bado haijakua, lakini pia anaweza kupoteza mwelekeo ikiwa chama alichokishabikia hakitashika dola huenda ikamwathiri pia vilevile kwa kukosa fursa nyingi na kuwekwa pembeni katika kila shughuli,” anasema Kitime.
Anasema hata hivyo kizazi cha sasa kimekuwa huru kujipambanua ukilinganisha na enzi zao. Kitime anaweka wazi kwamba huenda ndiyo sababu ya wanamuziki wakongwe kushindwa kujihusisha na masuala ya kisiasa kwa hivi sasa.
Naye mwimbaji mkongwe wa Kilimanjaro Band aka Wana Njenje, Waziri Ally anasema hashangazwi na wanamuziki wa zamani kutoshiriki katika masuala ya kisiasa kwa sasa, kwani anaamini kwamba wao walikuwa msatari wa mbele enzi za ujana wao hivyo wamewapa vijiti wasanii wachanga.
Anasema tofauti iliyopo baina yao na wasanii wa sasa ni mfumo wa vyama ambapo wao ilikuwa ni chama kimoja.Waziri anasema enzi zao wasanii walitumika kuhamasisha, kuburudisha na kusherehesha zaidi lakini wa miaka ya sasa amezidi kujipambanua na kwake haoni kama ni tatizo bali ni faida na maendeleo kwa tasnia ya sanaa nchini.
“Tulichokifanya sisi zamani ilikuwa kukusanya watu ili wanasiasa wafikishe agenda zao kisiasa, miaka ya sasa na wao wameingia katika siasa na wananchi wamewakubali hivyo tumesonga ni maendeleo,” anasema Waziri Ally.
Hata hivyo anafafanua kwamba hasara zipo japokuwa si nyingi sana, anasema inaweza kutokea mashabiki wakagawanyika kutokana na namna msanii anavyojipambanua.
lakini anaamini kwamba kuna uwezekano mkubwa wakarudi na kuipenda sanaa anayoitengeneza msanii ikiwa itakuwa bora.
Akizungumzia haki ya msanii kushiriki katika masuala ya kisiasa, Mkurugenzi Ukuzaji Sanaa na Masoko Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Vivian Msao Shalua anasema suala hilo halina athari yoyote kwa msanii na ni moja ya kazi zake.
“Kazi ya msanii ni kuburudisha, kuhamasisha, kuhimiza amani na upendo na kuwahamasisha wananchi kupiga kura ila tu anatakiwa asitukane na wala asivunje sheria yoyote ya nchi. Kinachotakiwa aimbe na kuhimiza wengine katika yale yaliyo sahihi na si kugombanisha chama kwa chama wala jamii na jamii,” anasema Shalua.