WAMEDATISHWA au wamekurupuka? Ndivyo unavyoweza kuhoji kutokana na kasi waliyonayo wasanii katika kuchangamkia siasa wakijitosa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Wasanii wa uigizaji, waimbaji na wengine wameuchangamkia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2015 na baadhi yao wamepenya kwenye kura za maoni na wengine kwenda na maji baada ya kukatwa.
Irene Uwoya alifanikiwa kupenya kupitia CCM viti Maalumu Vijana Mkoa wa Tabora, Mohammed Mwikongi ‘Frank’ yeye amepeta kupitia ACT, Joseph Haule ‘Prof Jay’ na Afande Sele wamepenya mkoani Morogoro kupitia vyama vya Chadema na ACT, Keysher, Said Fella walipeta kupitia CCM.
Fella alikuwa akiwania udiwani, wakati Keysher alipenya kwenye ubunge viti maalumu walemavu mjini Dodoma.
Wema Sepetu, Wastara Juma, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’, Juma Chikoka ‘Chopa Mchopanga’ ni baadhi ya waliopigwa chini kupitia chama cha CCM, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’ yeye bado haijafahamika kama kapenya kupitia CUF au la.
Sugu
Safari hii kumekuwa na mwamko mkubwa kwa baadhi ya wasanii kujitokeza kujaribu bahati zao ikiwa ni mara ya kwanza kwa wasanii wa filamu kuchukua uamuzi mzito kuomba ridhaa kwa raia, watu wa muziki wao tayari wapo Bungeni.
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Vicky Kamata, Martha Mlata ni baadhi ya wasanii wa muziki waliofungua pazia la wasanii kutwaa viti vya ubunge tangu walipojitosa katika uchaguzi uliopita.
Kabla ya hapo alikuwapo marehemu Kapteni John Komba na kushinda kwa Sugu kunaelezwa kama ndiyo sababu iliyowaamsha wengine, kwani walihisi kumbe kila kitu kinawezekana kwa kuwa haikutarajiwa kama Sugu angepita kupitia upinzani na safari hii ameteuliwa tena kutetea nafasi yake.
Mwaka huu, wasanii wa filamu ‘Bongo Movie’ waliamua kujaribu bahati zao na kujitokeza kuomba ridhaa ya kuwa wabunge kupitia vyama va kisiasa huku wasanii wengi wakiomba kupitia CCM na wawili tu wakiomba kupitia vyama vya upinzani.
Frank ameomba ridhaa ya kupeperusha bendera kupitia chama kipya cha ACT na anagombea jimbo la Segerea, huku mchekeshaji Kingwendu’akigombea jimbo la Kisarawe kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF).
Walioomba kupitia CCM walikuwa ni wengi na kura hazikutosha hivyo walishindwa na wakongwe wa chama hicho na kufanya watu waamini kuwa kupata nafasi ndani ya chama hicho si kazi rahisi, pamoja na wasanii kuwa na mvuto katika kukusanya watu, ila suala la kura za maoni ni changamoto.
Wema
Wema Sepetu mrembo wa Tanzania 2006 aliwania ubunge wa viti maalumu Singida mjini na kuchuana na wakongwe katika chama hicho na kujikuta akianguka na kuikosa nafasi hiyo, baada ya kuchukuliwa na Asharose Mateme. Wema alifanikiwa kushika nafasi ya nne.
Hali pia haikuwa shwari sana kwa Wastara Juma ‘Stara’ baada kujitosa mkoani Morogoro kuomba ridhaa ya CCM viti maalumu kupitia walemavu naye alipigana na kuangukia nafasi ya pili.
Kimbembe kilikuwa Jimbo la Kinondoni, msanii na mchekeshaji mahiri katika filamu Steve Mengere ‘SteveNyerere’ aliingia kupambana na vingunge na kura hazikutosa na kumjengea jina kisiasa.
Msanii huyo amesema kuwa amefarijika sana baada ya kugundua kuwa anakubalika na jamii anahitaji kupambana na changamoto zilizomfanya ashindwe ikiwa ni mbinu za kisiasa na kwamba ana imani anaweza kufanya vizuri na hataacha kugombea uongozi mbalimbali kwani anaweza.
“Nimekuwa kisiasa na nitaendelea kugombea uongozi kwani natosha ila kura hazijatosha kwa sasa, na hii inatokana na wananchi kuishi kwa mazoea kuwa kuna dhana kuwa vijana hatuwezi kuongoza lakini si kweli tunaweza tukipewa nafasi,”alisema Steve.
Irene
Msanii wa Bongo Movie Irene Uwoya aliibuka kidedea UVCCM-Tabora kwa hatua za awali lakini hakuweza kufua dafu katika mchujo uliofanyika mjini Dodoma ambako jina lake limekatwa.
“Nimeweka kambi huku na kuzunguka kila sehemu katika kujua matatizo ya wananchi wa Tabora kwani nimepanga kuwafanyia makubwa hususan vijana, naishukuru kampani yangu, Mike Sangu na Johari tumejipiga,” alisema Uwoya kabla hajakatwa katika hatua ya mwisho mjini Dodoma.
Nje ya Dar
Baada kutumiwa katika kampeni na shughuli mbalimbali za kisiasa, wasanii wa filamu walijipima kama wanaweza kwa kuwa ni vivutio kwa wapiga kura kwani mara nyingi wagombea wamekuwa wakiwaita na kuwapandisha majukwaani kabla ya wagombea kumwaga sera zao.
Wasanii wengi wa filamu walitoka nje ya Dar es Salaam wakiamini kuwa mapokezi wanayopewa na mashabiki wao yanaweza kuwa ni mtaji kwa wapiga kura, lakini inaonyesha ndani ya siasa kuna mbinu tofauti ili upigiwe kura ambazo wasanii wetu wamezikosa.
Hata hivyo, baada ya Mwanaspoti lilipozungumza na baadhi ya wasanii waliokwenda kugombea uongozi nje ya Jiji la Dar es Salaam imebainika kwamba wamekwenda kugombea katika sehemu za maisha yao.
Wengi wamekwenda sehemu walizozaliwa mama zao mfano, Wastara Juma Morogoro, Wema Sepetu Singida.
Naye Irene Uwoya akiwa na sababu kama hiyo hiyo kuwa mama yake naye ni mzaliwa wa Tabora. Hawa ni waliogombea kupitia viti maalumu ambao wote ni wa kike, lakini wasanii waliobaki ambao ni wanaume wamebaki Dar ambao ni Steve Nyerere, Mchopanga, Frank na Kingwendu.
Uzoefu
Suala la uzoefu nalo ni changamoto kwani kati ya hao wote ni msanii mmoja tu ambaye yupo katika chama kama kada na kiongozi zaidi ya miaka 10.
Msaani huyo ni Steve Nyerere ambaye amekuwa kamanda wa vijana katika Tawi la Bwawani lilopo Kata ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Watalamu wa masuala ya kisiasa wanaamini msukumo uliojitokeza kwa wasanii ulihitaji maandalizi ili kukabili ushindani uliopo ndani ya chama hicho chenye makada tofauti na vyama vya upinzani ambavyo upinzani katika kura za maoni hazina ushindani mkubwa.
Ushauri wasanii kwa sasa wanatakiwa kuimalisha taasisi, mashirikisho yao ambayo bado yanahitaji nguvu zao zinazohusu kazi za filamu na baadaye kuingia rasmi katika medani za kisiasa.