CCM wamedandia sera ya mafuta – M.Seif


Maalim-Seif--620x308
By Goodluck Eliona na Khelef Nassor
Zanzibar: Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema hakuna mwenye uhalali wa kuzungumzia uchimbaji wa mafuta ya Zanzibar zaidi yake. Alisema kuwa suala la mafuta ya Zanzibar ni ajenda yao na CCM wameidakia ni sawa na kudandia basi.
Suala la mafuta na gesi ambalo siku chache zilizopita lilikosolewa na Rais Jakaya Kikwete kuwa CUF haiwezi kulishughulikia ndani ya siku 100, Maalim Seif alisisitiza akichaguliwa atafanikiwa kutimiza lengo hilo kwa kuwa zipo nchi zilizoweza. “Rafiki yangu Kikwete sheria za mafuta mlizopitisha mapato yote yanakwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Zanzibar hainufaiki,” alisema.
Akizungumzia mpango wake atakapoingia madarakani, Maalim Seif alisema atajenga bandari mpya Unguja na Pemba, atapanua uwanja wa ndege na kujenga maghala makubwa ya kuhifadhia bidhaa. Pia, alisema anataka baada ya miaka mitano Zanzibar iwe na ajira nyingi kuliko ilivyo sasa ambapo vijana wanashindwa hata kuoa kwa kukosa ajira.
Alisema Serikali ya CCM imeshindwa kuwatafutia vijana ajira na kuwaacha wakihangaika. Katika mkutano huo, Mjumbe wa timu ya Kampeni ya CUF, Ismail Jussa Ladhu, Jussa ambaye pia ni Mgombea Uwakilishi kupitia CUF, Jimbo la Malindi, Mjini Unguja alisema inashangaza pale viongozi wa CCM, Zanzibar kujinasibu kuwa ajenda ya mafuta ni yao.