CCM yaahidi hospitali Ikungi na bandari kavu Manyoni

Info Post
8/31/2015 06:16:00 PM
Mgombea mwenza wa CCM, Bi. Samia Suluhu akiwahutubia wananchi katika mkutano wa kampeni ulofanyika Wilaya ya Ikungi.
Mgombea mwenza wa CCM, Bi. Samia Suluhu akiwahutubia wananchi katika mkutano wa kampeni ulofanyika Wilaya ya Ikungi.
MGOMBEA mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Samia Suluhu ameendelea kunadi ilani ya chama chake huku akiahidi ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi pamoja na ujenzi wa bandari kavu wilayani Manyoni endapo wananchi watakipa ridhaa ya kuunda serikali mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Bi. Samia alitoa ahadi hizo jana katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Ikungi, wilayani Ikungi ikiwa ni jitihada za serikali ya CCM kuhakikisha inaendelea kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi mjini na vijijini.

Alisema serikali watakayoiunda itaendelea kushughulikia kero ya maji katika vijiji vyenye ukame na kuhakikisha kila kijiji kinapata maji safi na salama kwa matumizi, pamoja na kuvipelekea umeme baadhi ya vijiji vya Singida Mashariki ambavyo bado vijafikiwa na huduma kupitia awamu ya pili ya mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kuchochea maendeleo vijijini. Alisema katika kuboresha miundombinu wataikarabati barabara ya Mung'aa kwenda Nkiku ili iweze kupitika na kuwasaidia wananchi wanaoitegemea barabara hiyo.

Akihutubia katika mkutano mwingine wa kampeni Wilaya ya Manyoni, Bi, Suluhu aliahidi ujenzi wa bandari kavu eneo hilo ikiwa ni jitihada za kuongeza nafasi za ajira kwa vijana na kukuza uchumi na maendeleo ya wilaya hiyo. Alisema Serikali watakayoiunda itaunda mfuko wa maji ambao utashughulikia kero za huduma za maji safi na salama kwa wakazi wake.

Aidha watahakikisha vijiji ambavyo bado havina mawasiliano vinapata huduma hiyo ili kuchochea maendeleo ya wananchi katika mawasiliano. Bi. Samia amewataka Watanzania kutofanya makosa ya kuvichagua vyama vingine vya upinzani maana havina muelekeo na kuviita vya kuunga unga.

"...Tusifanye mchezo kwa kuvijaribu vyama vya kuungaunga kuingia madarakani, huwezi kufanya majaribio ya kuonja simu...hivi mlisha ona wapi chama kinasimamisha wagombea ambao sio wao bali wameazimisha kutoka vyama vingine, hivi havitufai hata simu moja," alisema B. Samia Suluhu.