KAMA kawaida ya kolamu hii kuwaletea wasanii mbalimbali na kuwabananisha na maswali kedekede ambayo yamekuwa yakiwaumiza vichwa wasomaji wa gazeti hili kwa kushindwa kuelewa undani wake.
Alhamisi ya leo tunaye msanii wa filamu Bongo, Fatuma Ayubu ‘Bozi’ ambaye amefungukia mswali mbalimbali kama ifuatavyo:
Msomaji: Nakukubali sana hauna makuu, ila nilisikia umetembea na mastaa wengi, ni kweli na huwa unatumia kinga?
Bozi: Kama ulivyosikia ndivyo ilivyo, kinga ni muhimu huwa nazingatia sana hilo.
Msomaji: Ulipotaka kumpa gari msanii wa Bongo Fleva, Ally Nipishe akakataa ulilipeleka wapi?
Bozi: Kwa kuwa alikataa nililazimika kuliacha palepale kwenye yadi ya magari kwa sababu nilikuwa bado sijalilipia.
Msomaji: Dada mbona niliwahi kukuona ukipanda daladala maeneo ya Buguruni halafu unahonga gari, kwani hauna usafiri wa kutembelea?
Bozi: Kupanda daladala ni uamuzi tu, nilikuwa na usafiri kwa sasa sina.
Msomaji: Unajisikiaje kumuona Ali Kiba akiwa na Jokate? Nakumbuka uliwahi kusema Kiba ndiye mwanaume uliyempenda kuliko wengine wote uliowahi kuwa nao?
Bozi: Najisikia vibaya sana, mwanzoni nilikuwa nampenda mno Jokate lakini sasa hivi simpendi kwa sababu yupo na Kiba na ikitokea wakafunga ndoa naona nitakufa kwa presha.
Msomaji: Nakupongeza kwa uigizaji wako. Nilibahatika kuona filamu yako moja uliyocheza kama jini halafu nasikia kutembea na mastaa unaona fahari wakati mwingine unawatongoza na kuwahonga, ni kweli?
Bozi: Asante kwa pongezi. Nikwambie tu mimi sijawahi kumtongoza staa yeyote yule. Wenyewe ndiyo wananitaka, nahisi nina nyota kali.
Msomaji: Kinachonitatiza ni kitu kimoja, kwa nini huwa hushiriki kwenye shughuli za wenzako, ukiwa na tatizo si watakutenga?
Bozi: Sipendi mikusanyiko ya watu, naepuka majungu, ila nitajirekebisha soon (haraka).
Msomaji: Nakufahamu vizuri Bozi mtoto wa Ilala, najua uliolewa na una mtoto mmoja. Nilisikia ndoa ilikushinda kwa sababu ulikuwa mchepukaji, ni kweli?
Bozi: Si kweli, mume wangu niliachana naye kwa sababu alikuwa hajatulia. Pia alikuwa akinipiga mara kwa mara.
Msomaji: Napenda nikupe pole kwa kufiwa na pedeshee wako aliyekuwa anaishi Ilala wiki iliyopita. Ilikuwa bado kidogo yakufike ya msanii mmoja wa kike Bongo, mwanaume alitaka akufie ndani ukamkimbia, ni kweli?
Bozi: Si kwamba nilimkimbia, ukweli nilikuwa naye akaumwa ghafla nusu ya kufa. Ila kuepusha matatizo akaniambia niondoke, asije akanifia. Ndipo kesho yake nikaambiwa amefariki dunia. Namshukuru Mungu maana huenda yangenifika makubwa.
Msomaji: Kwa nini mlipigana na msanii mwenzio Kunguru kisa kikiwa kumgombea Nay wa Mitego, huoni kama mlijidhalilisha?
Bozi: Sababu yule ni rafiki yangu na alinivunjia heshima. Ilikuwa lazima nimfundishe adabu, ila najilaumu sana kwa nilichokifanya.
Msomaji: Wewe dada mbona ni mzuri kwa nini hutulii? Nakushauri utulie na bwana mmoja au huogopi Ukimwi?
Bozi: Asante kwa ushauri, nimeshatulia, hakuna asiyeogopa Ukimwi.
Msomaji:Napenda nikufahamu kwa kina, ulianza sanaa lini na mpaka sasa una filamu ngapi?
Bozi:Nilianza sanaa mwaka 2007 kwenye kundi la Mr. Chuz (Jumanne Kihangala) na filamu nilizocheza zipo nyingi, zikiwemo Mkoba wa Babu, Gundu na Hostel.
Chanzo: GPL