STAA wa sinema za Kibongo, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ hivi karibuni alinusurika kifo baada ya kula chakula chenye sumu na kulazimika kukimbizwa katika Hospitali ya Hurbert Kairuki Memorial iliyopo Mikocheni jijini Dar, Amani linakupa ripoti kamili.
Kwa mujibu wa chanzo, Steve alifika hotelini (jina linahifadhiwa) kupata chakula cha jioni na marafiki zake ambapo baada ya kula kidogo akaanza kulalamika tumbo linamuuma.
“Baada ya kula chakula alianza kushika tumbo na kulalamika kwamba alisikia kizunguzungu ndipo wenzake wakambeba na kumkimbika Hospitali ya Kairuki akiwa hajitambui,” kilisema chanzo.
Amani lilipopata taarifa hiyo, lilikwenda katika hospitali aliyolazwa msanii huyo kwa lengo la kujua afya yake ambapo alifungukia tukio hilo kwa masikitiko kwamba ilikuwa lazima afe.
“Hadi hapa nilipofikia kiukweli namshangaa sana Mungu kwani ilikuwa lazima nife. Nimekimbizwa hospitalini nikiwa sijitambui na nilipochomwa sindano za kitovuni zaidi ya tano, kidogo nikapata ahueni,” alisema Steve.
Steve aliruhusiwa hospitalini hapo juzi (Jumanne) mchana, kwa sasa anaendelea na dozi.
Chanzo: GPL