Watu wawili, Moris Thomas na Kobero Peter wamefariki dunia na mwanamke mjane mwenye watoto 10, Mwashamu Hassan amepooza ikidaiwa kuwa ni baada ya nyuma zao kuwekewa alama X. Wote ni wakazi wa Mtaa wa Kigogo, Mbuyuni, Kinondoni.
Tukio hilo lilitokea Jumatatu iliyopita na ilidaiwa kuwa marehemu hao na mama huyo walipatwa na mshtuko ghafla kuanguka. Kobero alipoteza maisha papohapo na Moris alipelekwa katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu ambako alikaa kwa siku moja lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya na kuhamishiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU),
Muhimbili ambako alifariki dunia Jumanne asubuhi. Mjane apooza Akisimulia mkasa huo juzi akiwa amekaa kwenye kipande cha godoro nyumbani kwake, Mwashamu alisema baada ya kuona nyumba yake ikipigwa X, alipatwa na mshtuko na kupooza ghafla kuanzia kiunoni hadi miguuni na kwamba hawezi kutembea tena. Alisema amekuwa akiishi katika nyumba hiyo aliyoijenga na marehemu mumewe Omary Hassan kwa miaka 15 sasa.
“Hii nyumba nimeijenga na mume wangu kwa kudunduliza pesa, nikiuza karanga yeye akifanya vibarua... tumeijenga kwa Sh12 milioni,” alisema. Alisema alikuwa akiishi kwa kutegemea nyumba hiyo yenye vyumba sita vya wapangaji na viwili alivyokuwa akiishi na watoto wake.
“Kila mwezi nilikuwa napokea Sh30,000 kwa kila chumba kutoka kwa wapangaji, sikuwa anapokea kodi ya miezi sita wala mwaka,” alisema. Mmoja wa watoto wa mama huyo, Ibrahimu Hassan alisema ilikuwa saa 3.35 asubuhi wakati wanakunywa chai waliposhangaa kuona kundi la watu wakiwamo askari wenye bunduki waliokuwa na chupa ambazo walikuwa wakizipuliza ukutani na kuandika neno “Bomoa”. “Tulibaki kushangaa hatujui nini kinaendelea, tuliuliza kuna tatizo gani tukaambiwa tunatakiwa kubomoa nyumba zetu, baada ya kusikia hivyo mama alianza kulalamika anajisikia vibaya,” alisema Hassan; “ilibidi tumnyanyue kumuingiza ndani ili asione kinachoendelea, tukashangaa kufika jioni mama hawezi kusimama wala kutembea.
” Hassan alisema kabla ya hali hiyo mama yao alikuwa anafanya kazi ndogondogo licha ya kuteguka mgongo kutokana na ajali na kuwekewa vyuma ambako alipewa masharti na madaktari ya kutofanya kazi nzito wala kupata mshtuko wa aina yoyote. “Tayari mama ameshapata tatizo, hapa unavyoona tangu tukio hilo litokee hawezi kutembea, wapangaji wote wamehama, wengine walitakiwa kutulipa kodi tarehe 13 mwezi huu lakini haiwezekani,” alisema. Hassan alisema kutokana na hali ngumu ya maisha yeye na ndugu zake hawana kipato cha kumsaidia mama yao.
“Wengi wetu tumeishia darasa la saba, tunafanya vibarua vidogo kumsaidia mama kupata pesa ya kula na kusomesha wadogo wetu,” alisema. Majirani Majirani wa mama huyo wamemlilia Rais John Magufuli wakitaka awaonee huruma wananchi wake akiwamo mjane huyo ambaye sasa amepata maradhi yaliyosababishwa na bomoabomoa. “Magufuli ulisema unampenda Mungu na unawapenda watu maskini,” alisema Saumu Mohamed huku Juma Mkude akisema:
“Kama hivyo unavyomuona ni mama wa watoto 10, wengine bado ni wadogo watakwenda wapi?” Mjumbe wa nyumba kumi, Maya Hatibu alisema: “Hali yake kama unavyomuona, hawezi kutembea tena mwenyewe alikuwa anafanya vijikazi vidogovidogo vilivyokuwa vikimwingizia kipato cha kila siku.” Nyumbani kwa Moris Akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa Moris iliyofanyika nyumbani kwake Kigogo Mbuyuni kabla ya kusafirishwa kwenda Kijiji cha Matombo, Morogoro alikozaliwa, kaka wa marehemu, Colneus Thomas alisema mdogo wake alikuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu